Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, kitengo cha habari cha Ataba Tukufu ya Alawi kimetangaza mkusanyiko wa ratiba za Wiki ya Idi ya Ghadir Khum katika awamu yake ya kumi na tano na kuchapisha maelezo ya programu hizi ambazo zitafanyika ndani na nje ya Iraq; miongoni mwa muhimu zaidi ni kupandishwa kwa bendera ya Eidullah al-Akbar nchini Iraq na kwenye mataifa mbalimbali duniani kupitia maeneo 150.
Khadim Haider Rahim, mkuu wa kitengo cha habari, katika mkutano wa waandishi wa habari uliohudhuriwa na kundi la waandishi wa habari kutoka vituo vya televisheni vya satelaiti, vyombo vya habari, mashirika ya habari pamoja na watengenezaji wa maudhui, alisema: “Programu za Wiki ya Kimataifa ya Ghadir zinafanyika kwa lengo la kuimarisha maadili ya kushikamana na Wilayah ya Amirul-Muuminina (as), na zinajumuisha programu za kidini, Qur’ani, kiutamaduni, kisanii, za wananchi, za huduma na kibinadamu, pamoja na programu mbalimbali maalumu kwa watoto.”
Rahim alifafanua: “Miongoni mwa programu muhimu zaidi ni kupandishwa kwa bendera ya mnasaba huu wenye baraka katika maeneo 150 na mikusanyiko ya sherehe ndani na nje ya Iraq; ikiwemo katika nchi za Ulaya, nchi za Kiarabu na Kiislamu, katika mikoa yote ya Iraq, katika Ataba Tukufu na maeneo matukufu ya ziara, pamoja na maeneo kadhaa katika mji wa Amirul-Muuminina (as), Najaf Ashraf.”
Pia alieleza kuhusu programu maalumu ya kupandisha bendera hii yenye baraka katika miji 21 ya Iran ambayo imekuwa shabaha ya mashambulizi ya Kizayuni na Marekani, na akasema kuwa; programu hiyo itaambatana na mpango wa kutoa huduma na kusaidia familia za wahanga wa janga la shule ya mji wa Minab; hatua ambayo inafanyika katika mfumo wa mpango wa kibinadamu na mshikamano ambao Ataba Tukufu ya Alawi ilikuwa imetangaza hapo awali kupitia kampeni yake ya misaada kwa taifa la Iran, ili kufikisha ujumbe wa matumaini na kuwa ishara ya maana za kushikamana na Wilayah pamoja na kuhusika na maadili ya Ghadir Khum.
Mkuu wa kitengo cha habari cha Ataba Tukufu ya Alawi alisisitiza: “Wiki ya Kimataifa ya Ghadir pia itashuhudia kufanyika kwa maonesho ya tamthilia yatakayoshirikisha waigizaji 500 kwa muda wa siku 15 katika eneo la mapumziko la Nakhilat; mahali ambapo pana uwezo wa kuchukua zaidi ya watu 5000. Aidha, kutakuwa na shughuli za kijamii, sherehe za ndoa kwa wahitaji, programu za kitamaduni na kielimu, pamoja na sherehe mbalimbali zitakazofanyika katika maeneo 16 ya mji wa Amirul-Muuminina (as), Najaf Ashraf.”
Inafaa kutajwa kwamba programu za Wiki ya Ghadir Khum zimeanza Jumatatu, kwa kupandishwa bendera ya Eidullah al-Akbar kandokando ya Haram Tukufu ya Amirul-Muuminina (as), na wakati huohuo bendera hiyo yenye baraka itapandishwa pia katika Ataba Tukufu, maeneo matukufu ya ziara, mikoa ya Iraq na mataifa mbalimbali duniani; ikiwa ni ishara ya kuanza kwa shughuli za kuadhimisha Idi ya Ghadir Khum, Idi ya kuifanya upya ahadi ya utiifu na Wilayah kwa Amirul-Muuminina (as).
Maoni yako